Makamu wa pili wa Rais wa serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Ndugu Hemed Suleiman Abdulla amezitaka pande mbili zilizokuwa na mgogoro wa mpaka kati ya Wilaya ya Kilindi mkoani Tanga na Kiteto mkoani Manyara kuridhia mpaka uliowekwa na serikali kwa lengo la kumaliza mgogoro huo uliodumu kwa muda mrefu
Akizungumza katika kikao na wanachama wa Chama cha Mapinduzi Ndugu Hemed ambaye pia ni mlezi wa CCM mkoa wa Tanga alisema Mh Rais Dk Samia Suluhu Hassan ametimiza jukumu lake la kumaliza mgogro huo na kilichobaki ni wananchi wa pande mbili hizo Wilaya Kilinid na Kiteto pamoja na wakazi wake kutimiza majukumu yao ambayo ni kuhakikisha mgogoro hautakuwepo tena
Alisema maeneo yenye migogoro ya ardhi yana tija ndogo katika maendeleo na katika kipindi chote cha mgogoro kunakuwa hakuna faida yeyote zaidi ya athari mbalimbali zenye kuleta hasara kwa jamii
Makamu huyo wa pili wa Rais wa serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar alisema suala la amani ni muhimu na ndio msingi wa maendeleo katika jamii yeyote.
Ndugu Hemed alisema Chama cha Mapinduzi kimekuwa kikihimiza suala la amani na utulivu kwa watanzania wote na kuwataka viongozi katika ngazi zote kushirikiana kutoa elimu ya umuhimu wa kuishi pamoja kwa amani
Akizungumzia kuhusu uchaguzi wa serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika mwezi Novemba 27,mwaka 2024 Ndugu Hemed aliwataka wanachama wa CCM na viongozi wa chama hicho kuhakikisha chama chao kinashinda katika uchaguzi huo
Aliwataka wanachama wa CCM wenye sifa kujitokeza kuomba nafasi za uongozi katika uchaguzi huo na kutoa wito kwa wanaopitisha majina ya wagombea uongozi kupitisha majina ya watu ambao watakwenda kuwatumikia wananchi na si vinginevyo
Kuhusu changamoto ya barabara Mlezi huyo wa chama mkoani Tanga aliahidi kuiwasilisha changamoto hiyo sehemu husika ili itatuliwe na kuwahakikishia wanakilindi kuwa ipo siku changamoto hiyo itakuwa ni historia katika wilaya Kilindi
MODI MNGUMI
Copyright ©2018 Kilindi DC . All rights reserved.